Thursday 27 September 2007

Msimamo Wetu

SDP ni chama cha mapinduzi. Tunapambana kupindua mambo yote maovu na ya kupinga maendeleo na kuleta mambo mema na ya kimaendeleo nchini na duniani. Tunaamini kuwa barabara ya ukombozi kamili wa umma ni ya kimapinduzi. Na mwanzo wa mapinduzi yetu ni kujikomboa kimawazo ili tuweze kujiamini kama Wakenya, kama Wafrika, kama watu weusi na kama watu hasa. Hakuna kutawalwa kubaya kuliko kutawalwa kimawazo. Ndiyo kwa maana SDP tunapinga kasumba ya kikoloni ati sisi watu weusi hatukuwa tunafanya historia kabla ya ukoloni. Tunapinga uongo ati mila na tamaduni za Wakenya, Wafrika na watu weusi ni za kishenzi na za kupinga maendeleo. Hatukubali ati sisi watu weusi tunastahili daima kuwa makasuku wa kuiga lugha, mila, desturi na tamaduni za kigeni. Tunachukia kugeuzwa watu wa kuhurumiwa, kutegemea na kuishi kwa misaada, mikopo na mitumba ya vitu na mawazo. Wakenya tunaweza kujiamulia sudi yetu sisi wenyewe. Tunakataa uongo ati wakoloni walivamia nchi yetu ili kututoa kwa ushenzi na kututia kwa ungwana, na ati kabla ya wa wageni kuja huku hatukuwa tumegundua chochote cha maana. Si kweli ati ukoloni-mamboleo upo Kenya kwa masilahi ya maendeleo ya Kenya. SDP tutaendelea kuzingatia, kushikilia na kusambaza urithi wetu wa kitamaduni wa kimaendeleo kutoka kwa mabibi na mababu zetu. Wakati wote tutapambana dhidi ya kasumba ya kikoloni inayoenezwa na wakoloni na vibaraka wao nchini. Tutapigana na chochote kile kinachopinga uhuru wetu na kuparaganya historia na utamaduni wa mtu mweusi na wa wanaonyonywa na kugandamizwa. Tunapinga porojo za wadhalimu ati mfumo wa kunyonyana na kugandamizana ni wa halali na ati hauwezi kuepukika. Kwani tunafundisha elimu ya ukombozi wa wengi, elimu ya kiutu ya kujaili binadamu wengine, elimu ya matumaini ya ukweli na maisha ya furaha kwa wengi wanaonyanyaswa. Tunaamini umma. Umma ndiyo hufanya historia. Umma wa wanyikazi na wakulima ndiyo wenye uwezo na jukumu la kuongoza harakati za kuondoa dhuluma za mfumo wa ubepari-ukoloni-mamboleo. Umma wa Kenya ndiyo kiini cha mapinduzi ya kuboresha maisha ya jamii ya Kenya. Ndiyo kwa maana SDP ni Chama cha kweli cha umma wa Kenya.

SDP kama idadi kubwa zaidi ya Wakenya, na msingi wetu ukiwa kwa umma, tunachukia utawala wa kiimla kwani tunashuhudia hasara yake kila siku. Ndiyo kwa maana tutaendelea kujitoma katika msitari wa mbele wa harakati za kuleta uhuru, demokrasi na haki za binadamu. Kwa msingi huu, siku zote tutapambania na kulinda uhuru wa kukutana, kutoa maoni, kuandamana na wa imani. Tutapigania na kutetea uchaguzi huru na wa haki wa madiwani, wabunge na rais. Tunazingatia demokrasi ya mfumo wa vyama vingi bali demokrasi inayowapa umma uwezo kutoka mashinani wa kushiriki kikamilifu katika mambo yote muhimu yanayohusu maisha yao ya kila siku, mkiwemo umilikaji, uzalishaji na ugamvi wa rasilimali za kitaifa. Tutashirikiana na watu wote, wawe kwa chama, kikundi ama binafsi, ambao wanashikilia msimamo huu.

SDP ni chama cha wazalendo, tena wazalendo wakereketwa. Tunapenda Kenya yetu, tena sana. Tuna uchungu mkubwa na taifa letu. Ndiyo kwa sababu tunashirikiana na tutaendelea kushirikiana na watu wote wanaotaka kuona ukombozi wa kitaifa na maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni nchini. Tunapinga ubepari, ukoloni-mamboleo na chochote kile kinachopinga uhuru, ukombozi na maendeleo ya taifa letu. Tunakataa ukabila, ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kijinsia, ubaguzi wa kiumri na chochote kile kinachohatarisha umoja wa Kenya na kuzuia maendeleo yetu. Tutapambania haki ya kila Mkenya kuishi na kuwa na mali pahali popote pale anapochagua nchini. Tutakuwa katika msitari wa mbele wa kufichua na kupambana dhidi ya njama zozote zile zenye lengo la kupanda mbegu za chuki na uhasama miongoni mwa makabila ndugu ya Kenya. Kwani Kenya tuipendayo ni ya amani, salama, uhuru, utangamano na maendeleo ambapo kila mtu anaishi maisha ya kiutu bila kunyonywa, kugandamizwa na kubaguliwa kwa vyovyote vile. Ndiyo kwa maana tunapambania Katiba Mpya ya Kitaifa itakayozingatia na kuhakikisha, miongoni mwa mambo mengine, usambazaji wa mamlaka ili kuhakikisha kuwa kila sehemu na kabila itakuwa na mamlaka ya kushiriki katika kusimamia na kufaidi kutoka kwa rasilimali zilizoko karibu nao. Usambazaji wa uongozi utahakikisha kuwa wananchi wanashirikishwa kujiamulia jinsi ya kuendesha maisha yao ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii kutoka mashinani na maamuzi ya kutoka chini hadi juu ya kushirikisha watu wote.

SDP tunakataa mfumo wa ubepari kwani ni mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu. Na mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu ni mfumo wa kinyama - wa mwenye nguvu mpishe mnyonge msonge. Mfumo huu wa kijamii-kiuchumi unaotawala Kenya tangu uhuru umekuza adili za kishenzi za ulafi, ufisadi, wizi, ukatili, udhalimu, kuoneana, kunyang’anyana, kushindana kama wanyamapori, kupunjana na kudanganyana. Mfumo huu wa unyanyasaji ni kinyume cha utamaduni wa kimaendeleo wa Kiafrika, na wa ubinadamu, unaozingatia maadili ya kiutu ya usawa, umoja, kusaidiana, huruma, mapenzi, urafiki na bidii. Hivi sasa matajiri wachache sana wanazidi kutajirika huku idadi kubwa zaidi ya wananchi wanazidi kufukarika. Pengo kati ya wenye mali na walalahoi linapanuka usiku na mchana. Ufisadi umekithiri na kuwa donda ndugu. Wafanyikazi wameporwa haki zao, wananyonywa na kugandamizwa na waajiri kiholela. Wanaotoa jasho wanaishi kama watumwa huku ambao hawafanyi kazi wanaishi kwa anasa na starehe za kifalme. Wakulima wadogo hawafaidi kutoka kwa juhudi zao za kilimo kwani mazao yao yanadhibitiwa na walanguzi wanaolindwa na nguvu za dola. Mfumo huu wa kinyama umefanya Kenya kuwa na aibu ya kuwa na wananchi wasio hata na inchi ya nchi yao, maskwata! Msingi wa ujambazi, wizi, unyang’anyi, umalaya, ufisadi, vita nyumbani na maovu yote yanayoguguna jamii yetu, ni mfumo huu wa kupinga ukombozi wa wengi. Hakika hatuwezi kuishi kwa amani, usalama, utu na ungwana chini ya mfumo wa ubepari unaolinda kunyonyana na kudhulumiana.

SDP tunapendelea mfumo wa kisoshalisti, mfumo wa kiutu ambao kinadharia na kimatendo unapigania ukombozi wa kila anaenyonywa na kugandamizwa. Mfumo wa kisoshalisti utahakikisha kuwa kila mwananchi anafaidi na kufurahia rasilimali za taifa. Tunapendelea mfumo wa kisoshalisti kwani utatengeneza hali ya kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye afya anafanya kazi na kula matunda ya jasho lake. Tunapambania mfumo wa kisoshalist kwani unazingatia masilahi ya kiutu ya kila mtu, mkiwemo watoto, wazee, wagonjwa na walemavu. Mfumo wa kijamii-kiuchumi tunaoutaka ni ule unaoshikilia maadili ya usawa, haki, umoja, huruma, kusaidiana, kugawiana na utekelezaji wa haki za binadamu si kwa maneno tu bali kwa vitendo. Tunahubiri kuhusu mfumo utakaokomboa jamii ya Kenya kutoka kwa hali iliyopo ya unyama wa kunyonyana, kunyang’anyana, kushindana, kuoneana, kupunjana na kudanganyana. SDP tunajua ukweli kwamba Kenya ina rasilimali za kutosha kumwezesha kila mwananchi kuishi maisha ya kiutu na kimaendeleo, bora tu tuondoe utamaduni wa choyo na tamaa za kinyama. SDP tunatambua ukweli kuwa bila nadharia ya kimapinduzi hapawezi kuwa na harakati za kimapinduzi. Ndiyo kwa maana tunazingatia na tutazingatia nadharia ya kisoshalisti ambayo itatumulikia barabara sahihi ya kujenga jamii ya kisoshalisti Kenya.

SDP tunaamini ukweli kuwa maendeleo ya Wakenya yataletwa na Wakenya wenyewe. Uhuru na ukombozi wa Kenya unatutegemea sisi wenyewe. Ndiyo kwa maana tunazingatia siasa ya ujamaa na kujitegemea. Historia ya Kenya na Afrika hadi sasa imetufundisha kuwa hatutakanyaga barabara ya maendeleo kwa kutegemea misaada na mikopo ya wale wale wanaoutunyonya na wanaotufukarisha. Wala hatutakombolewa na mawazo ya kibeberu ya kutudunisha na kutushindilia katika mfumo wa kibepari-kikoloni. Umaskini nchini hautaondolewa na sera za kiuchumi za kudhulumu wa wafanyikazi kama ubinafsishaji wa mashirika ya umma, uhuruishaji wa uchumi, kwa ufupi ubeparishaji wa kila sekta ya uchumi. Tutakuwa watu wa mitumba ya mabeberu hadi lini? Tutajiamulia sudi yetu wenyewe siku gani? Kwa nini tusijifikirie na kujifanyia sisi wenyewe? Si tu watu kama watu wengine? SDP tunazingatia ukweli kwamba tukifanya kazi kwa bidii na kuhakikisha tunakula matunda ya jasho letu sisi wenyewe; tukitumia rasilimali zetu vizuri huku tukihakikisha zinafaidi kila mwananchi; tukiwa na demokrasi ya umma; tukiwa na viongozi wa kizalendo wenye makini na wanaozingatia masilahi ya taifa; tukihifadhi mazingira yetu; tukiwa na sera sahihi za kiuchumi na kisiasa – ya kisoshalisti; Kenya itakuwa katika barabara ya uhuru na maendeleo. Haya tunayaamini kwa maneno na kwa vitendo, kwani hata sisi wa SDP hatukubali kuishi kwa uzembe na ulegevu, hatutegemei vya kupewa na wala hatuishi kwa uhalifu. Tunaishi kwa kulima na kufanya kazi, kwa kuhangaika na kushughulika usiku na mchana. Hatuketi na kulalamika tu, tunajaribu, tunajikaza kisabuni, tunapiga konde moyo kila mara. Msimamo huu ndiyo utatuletea uhuru na maendeleo.

SDP tunaunga mkono harakati za ukombozi wa Waafrika na watu weusi pahali popote walipo ulimwengini. Kwani tunafahamu historia chungu ya Wafrika na watu weusi ya kuwa chini ya utumwa, ukoloni-mkwengwe, ukoloni-mamboleo na ubepari. Tunafahamu njama za ubaguzi wa rangi zinazoendeshwa na ubepari na ubeberu dhidi ya Waafrika na watu weusi kote duniani. Tunajua kuwa sera za kiuchumi za kinyama za ukoloni-mamboleo zina njama za kuzuia na kuharibu uhuru na maendeleo ya Waafrika na watu weusi. Kwa sababu hii, tunaunga mkono muungano wa kimapinduzi wa Afrika. Tunakaribisha kwa mikono miwili Jumuia ya Afrika Mashariki na hatimaye kuwepo kwa taifa moja la Afrika Mashariki litakaloshirikisha Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na hata Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Lakini lazima muungano wa nchi za Afrika Mashariki na hatimaye Afrika uwe kwa ajili ya masilahi ya umma wa Mashariki na Afrika. Ndiyo kwa maana sisi tunaunga mkono harakati za kidemokrasi, haki za binadamu na kisoshalisti zinazoendelea Afrika na kote ulimwenguni. Kwani Wafrika na watu weusi hawawezi kuwa na uhuru, umoja, amani na maendeleo chini ya mfumo wa ubepari na ukoloni-mamboleo. Barabara ya ukombozi wa Wafrika na watu weusi duniani ni barabara ya kimapinduzi, usoshalisti.

SDP tunajua kuwa ubeberu ni adui mkubwa wa uhuru na maendeleo ya umma wa Kenya na wa dunia. Chini ya ubeberu, leo kwa sura ya ukoloni-mamboleo, nchi yetu inatawalwa kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kimawazo na hata kijeshi. Uchumi mkubwa wa viwanda, nishati, fedha, biashara kuu ya ndani na nje na hata mashamba mengi makubwa unadhibitiwa na mataifa ya kigeni. Rasilimali za nchi yetu zinatumika kujenga mataifa mengine huku nchi yetu ikididimia kwa lindi la umaskini kila kuchako. Jasho la wafanyikazi na wakulima wa Kenya linatumiwa kuzalishia wakoloni-mamboleo na vibaraka wao utajiri wa ajabu huku idadi kubwa ya Wakenya ikizidi kuangamia kwa umaskini na kutegemea misaada na mikopo kutoka kwa ubeberu ule ule. Hakika hatuwezi kuona uhuru wa kitaifa wakati ambapo tuko chini ya makucha ya ubeberu. Yoyote yule anaeunga mkono ubeberu ni adui wa uhuru, maendeleo na ukombozi wa Kenya. Serikali inayounga mkono ubeberu ni serikali ya kisaliti. SDP tutashirikiana kwa hali na mali na yoyote yule anaepinga ama kupambana dhidi ya ubeberu na ndiyo kwa sababu tunaunga mkono Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.

SDP tunapinga vikali ufisadi. Kwani ufisadi: uporaji wa mali ya serikali na ya umma, utumiaji madaraka vibaya, ubakuaji wa mashamba na maploti ya umma, utoaji na ulaji rushwa, wizi na uporaji unaofanywa na viongozi, magendo, ulanguzi, umafia - yote haya yanachangia kupinga maendeleo na ukombozi wa Kenya. Ufisadi unavunja nyoyo za watu wa bidii na waaminifu huku ukihujumu juhudi za Wakenya za kuboresha maisha yao. Tunajua kuwa kuna idadi kubwa ya matajiri nchini ambao wamepata utajiri wao kutokana na ufisadi. Wakati huo huo umma wa Wakenya unateseka kwa dhiki na shida za kila aina kutokana na ufisadi ambao sasa umekuwa dondandugu. Wengi wanakufa kutokana na ufisadi. SDP tunaamini kuwa serikali yoyote ile inayolinda ama kuongozwa na watu wanaofanya ufisadi haistahili kuwa madarakani. Vilevile, serikali ya kidemokrasi inayoongozwa na wazalendo na inayozingatia masilahi ya umma na ya kitaifa, haiwezi kushindwa kuumaliza utamaduni wa ufisadi. SDP tutakuwa katika msitari wa mbele wa mapambano ya kung'oa mizizi ya ufisadi nchini.

SDP siku zote tutapambania kuheshimiwa na kutekelezwa kwa haki za binadamu nchini na popote ulimwenguni. Kwani tunaamini kuwa kila binadamu ana haki ya kuishi maisha ya afya, amani, salama, furaha, shibe, kiutu na bila hofu wala wasiwasi. Binadamu wote ni sawa kwa mujibu wa kuwa binadamu. Hivyo, hakuna binadamu yoyote mwenye haki dhidi ya maisha ya binadamu mwingine. Wala hakuna mtu yoyote yule anaestahili kuteswa kwa sababu yoyote ile. Ndiyo kwa maana tunapinga hukumu ya kifo na uvunjaji wa haki za binadamu unaondelea ndani ya magereza ya Kenya na popote pale ulimwenguni. Tunalaani unyama unaofanywa na polisi dhidi ya raia. Tunapinga udhalimu wa aina yoyote ile mkiwemo ule wa wanaume dhidi ya wanawake. Tutatetea haki za kila mtu mkiwemo wazee, watoto, walemavu, wafungwa na wakimbizi. Tunakataa utamaduni wa hofu na kimya. Tunataka ule wa kidemokrasi. Watu waseme. SDP tunatoa mwito kwamba katiba mpya ya kitaifa iondoe sheria zote za kinyama na kufafanua, kuhakikisha na kulinda haki za binadamu wazi na bayana. Tena tunaamini kwamba hatua ya muhimu na ya kimsingi ya kuelekea kwa utekelezaji wa haki za binadamu ni kuondolewa kwa mfumo wa ubepari na ubeberu nchini na ulimwenguni.

SDP tu sehemu ya harakati za ukombozi wa jamii kutoka kwa ubaguzi wa kijinsia. Tunaamini kuwa wanawake na wanaume ni sawa na aidha hili sharti litekelezwe kwa maneno na vitendo. Tunatambua, kwa uchungu, kwamba katika jamii yetu wanawake, ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu, bado wananyanyaswa kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kwa kila hali na mfumo wa kibepari-ubeberu. Ndiyo kwa maana SDP tunaamini kuwa harakati za ukombozi wa jamii kutoka kwa unyanyasaji wa wanawake lazima ziende sambamba na harakati dhidi ya mfumo wa ubepari na ubeberu. Tunafahamu kuwa njaa, umaskini, ukosefu, unyonyaji, ujinga na ushenzi unaosababishwa na mfumo wa ubepari-ubeberu nchini ni kiini cha nyanyaso za kila aina. Tena katika jamii kama ya Kenya ambayo imegawanyika kitabaka, mapambano ya kuondoa unyanyasaji wa wanawake hayawezi kamwe kutenganishwa na harakati za kitabaka. Wala mapambano ya ukombozi wa wanawake si ya wanawake pekee bali ni ya wanawake na wanaume wapenda haki na maendeleo. SDP tushikilia kwamba mojapo wa mizani muhimu ya kupima kiwango cha uhuru na maendeleo katika jamii ni kiwango cha ukombozi wa wanawake katika jamii. Mfumo wa usoshalisti ndiyo msingi wa kujenga usawa wa kijinsia nchini na duniani.

No comments: